MAREKANI-SOMALIA-KENYA

Marekani yawafukuza Wasomali 67 na Wakenya 5

Ndege ya kibinafsi iliyowasafirisha raia wa Somalia na Kenya Mei 12 katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi
Ndege ya kibinafsi iliyowasafirisha raia wa Somalia na Kenya Mei 12 katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Wikipedia

Raia wa Somalia 67 na Wakenya watano wamefukuzwa nchini Marekani kwa nguvu baada ya kubainika kuwa walikuwa wanaishi nchini humo kinyume cha sheria lakini pia kujihusisha na makosa mbalimbali.

Matangazo ya kibiashara

Ndege ya kibinafsi iliyowabeba watu hao iliwasili katika uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Ijuma asubuhi.

Maafisa nchini Kenya wanasema walikuwa wanafahamu kuhusu kurejeshwa kwa raia wa nchi hizo mbili, na tayari  raia wa Somalia wamerejeshwa mjini Mogadishu kwa kutumia ndege nyingine  ya kukodi.

Hatua hii ilitarajiwa kutokana na operesheni inayoendelea nchini Marekani kuwarudisha nyumbani wahamiaji haramu wanaoishi nchini humo lakinia pia wageni wanaojihusisha na makosa mbalimbali.

Mwezi Januari ,wakenya wawili na raia wengine 90 wa Somalia walifukuzwa Marekani kwa sababu mbalimbali.

Rais Donald Trump miezi kadhaa iliyopita, aliamua kuwazuia wahamiaji kutoka mataifa ya Kiislamu kuingia nchini humo, hatua ambayo ilizuiwa na Mahakama.

Mataifa yaliyolengwa ni pamoja na Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen.