SUDAN KUSINI

Rais Kiir asema nchi yake ni salama hata baada ya kumfuta kazi Jenerali Paul Malong

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Jok Solomon

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema raia wa nchi hiyo wasiwe na hofu yoyote kuhusu usalama wao na badala yake waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya rais Kiir imekuja siku mbili baada ya kumfuta kazi Mkuu wa Majeshi nchini humo Jenerali Paul Malong.

Kupitia barua iliyochapishwa katika vyombo vya Habari nchini humo, rais Kiir ameeleza kuwa usalama wa nchi hiyo upo thabiti na hakuna haja ya raia wa nchi hiyo hasa wale wanaoishi  na kufanya kazi jijini Juba kuingiwa na hofu.

Aidha, Kiir amesema amekuwa katika mazungumzo na Malong ambaye amemhakikishia kuwa yuko salama na hivi karibuni atarerejea jijini Juba.

Wasiwasi ulizuka nchini humo baada ya kuripotiwa kuwa Jenerali Malong alikuwa ameondoka jijini Juba pindi tu baada ya kufutwa kazi na alikuwa na mpango wa kuanzisha uasi dhidi ya uongozi wa Juba.

Jenerali huyo hata hivyo alijitokeza na kusema kuwa hana nia yoyote ya kuanzisha uasi, na anachokitaka kwa sasa ni kupumzika na atarejea jijini Juba baadaye.

Raii Kiir alisema alimfuta kazi Malong ili kutoa nafasi kwa jeshi kupata uongozi mpya ambalo ni jambo la kawaida katika uongozi wa jeshi nchini humo.

Jeshi nchini Sudan Kusini limeendelea kushutumiwa kutekeleza mauaji ya raia na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makwao.