SUDAN KUSINI-UN

Umoja wa Mataifa unahitaji Dola Bilioni 1.4 kuwasaidia watu Milioni mbili Sudan Kusini

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa katika eneo la Tomping, jijini  Juba
Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa katika eneo la Tomping, jijini Juba Beatrice Mategwa/United Nations Mission in South Sudan (UNMISS)

Umoja wa Mataifa unasema inahitaji Dola Bilioni 1.4 mwaka huu kuwasaidia karibu watu milioni mbili waliomkimbia makwao kwa sababu ya vita na ukame nchini Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Shirika linaloshughulikia wakimbizi la UNHCR na lile la  mpango wa chakula duniani la  WFP  yalikuwa yamesema kuwa yalihitaji Dola Bilioni 1.2 lakini baada ya kuthathmini hali zaidi, imebainika kuwa fedha hiyo haitoshi.

Filippo Grandi Mkuu wa UNHCR amesema  hali mbaya ya kibinadamu inawafanya maelfu ya watu kuondoka nchini humo mara kwa mara.

Mapigano yamekuwa yakiendelea nchini humo tangu mwaka 2013, miaka miwili tu baada ya taifa hilo jipya duniani kupata uhuru wake kutoka kwa Sudan.

Maelfu ya watu wamepoteza maisha huku zaidi ya Milioni mbili wakitorokea katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Sudan, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais wa wa Sudan Kusini Salva Kiir  na kiongozi wa waasi Riek Machar anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini wamekuwa wakilaumiana kuhusu hali inayoshuhudiwa nchini mwao.

Wawili hao walishindwa kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2015 jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.