UGANDA-USALAMA

Acheni kuwatesa washukiwa, rais Museveni awaambia Polisi

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni REUTERS/James Akena

Rais wa Uganda Yoweri amewaandikia barua wakuu wa vitengo vya usalama nchini humo kuwaonya dhidi ya kuwatesa washukiwa wanaotuhumiwa kuhusika na  makosa mbalimbali nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Museveni ambaye ameongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, amesema njia hiyo haifai na haistahili kutumiwa tena nchini humo katika jitihada za maafisa wa usalama kutafuta ukweli kutoka kwa washukiwa.

Hatua hii ya kiongozi huyo imekuja baada ya kuwepo kwa ripoti kuhusu namna polisi wanavyowatesa washukiwa wa mauaji wa aliyekuwa msemaji wa Polisi Andrew Kaweesi aliyepigwa risasi mwezi Machi mwaka huu jijini Kampala.

Aidha, ameonya kuwa maafisa wa usalama wataendelea na mbinu hiyo, basi kuna uwezekano mkubwa watu wasio na hatia watafunguliwa mashtaka na kuwaacha wahusika.

Museveni ambaye ni mwanajeshi wa zamani, amewataka Polisi nchini humo kutumia mbinu za kisasa ikiwa ni pamoja na mfumo wa teknolojia kuwatafuta washukiwa wa makosa mbalimbali.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limeitaja nchi ya Uganda kuwa mojawapo ya nchi ambazo maafisa wake wa usalama wanawatesa washukiwa wa makosa mbalimbali na kukiuka haki zao.