KENYA

Serikali ya Kenya yashusha bei ya unga wa mahindi, wapenzi wa Ugali wafurahi

Sahani ya ugali, chakula kinachopendwa sana Afrika Mashariki
Sahani ya ugali, chakula kinachopendwa sana Afrika Mashariki Yutube

Serikali ya Kenya imetangaza kushusha bei ya unga wa mahindi baada ya kununua kiasi kikubwa cha mahindi kutoka nchini Mexico wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Kuanzia siku ya Jumatano, mifuko miwili ya unga itauzwa madukani kwa bei ya Shilingi 90 za nchi hiyo karibu Dola 1, na kuwapa afueni kubwa raia wa nchi hiyo.

Waziri wa Kilimo nchini humo Willy Bett ameeleza kuwa mfuko mmoja wa unga utauzwa kwa bei ya Shilingi 47, hatua ambayo imekubaliwa kati ya serikali na wasagaji unga.

Aidha, ameeleza kuwa serikali imetenga fedha za kutosha kuhakikisha kuwa inanunua mahindi mengine ikiwa yaliyopo sasa yatapungua katika siku za hivi karibuni. Chakula kikuu cha Wakenya wengi ni ugali.

Kupanda marudufu kwa bei ya mahindi ya kusaga na unga wa ugali, limekuwa suala tata nchini Kenya na kuzua mvutano wa kisiasa kati ya serikali na upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.

Mgombea wa urais kupitia muungano wa upinzani NASA Raila Odinga, amekuwa akihoji ni kwanini serikali ya rais Uhuru Kenyatta ilisubiri kumalizika kwa hifadhi yotey a mahindi katika maghala ya serikali kabla ya kuamua kununua tani 29,900 katika dakika za mwisho.

Hata hivyo, rais Uhuru Kenyatta ametetea hatua hiyo na kueleza kuwa sababu kuu ilikuwa ni kwa sababu walitoa nafasi kwa wakulima wa ndani kuiuzia serikali mahindi yao kabla ya kwenda nje ya nchi.

Pamoja na hilo, kumekuwa na mjadala kuhusu ikiwa kweli mahindi hayo yalinunuliwa nchini Mexico kwa sababu yaliwasili siku tatu katika bandari ya Mombasa baada ya serikali kuyaagiza.

Imeripotiwa kuwa, huenda mahindi hayo yalinunuliwa nchini Afrika Kusini wala sio Mexico kama inavyolezwa.

Licha ya mvutano huu, Wakenya wanasema wamepata afueni kuhusu bei ya unga baada ya kukosa kula mkate kwa kipindi kirefu.