EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo kwenye njia panda ?

Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwaka 2017 mjini Arusha nchini Tanzania
Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwaka 2017 mjini Arusha nchini Tanzania Wikipedia

Marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki watakutana jijini Dar es salaam nchini Tanzania  katika mkutano wao wa 18 kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili Jumuiya hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Ajenda kuu ya mkutano huo itakuwa ni kujadili ushirikiano "tata wa kibiashara" kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya EPA, lakini pia kuthathmini mchakato wa kuwepo kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Mkutano huu uliotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka huu, umeahirishwa mara tatu kwa sababu mbalimbali. Kwa kawaida, mikutano mikuu ya viongozi wa nchi hufanyika mara mbili kwa mwaka, mwezi Aprili na Novemba.

Viongozi hao watakutana wakati huu nchi wanachama kama Burundi na Sudan Kusini, zikiendelea kukabiliana na mvutano wa kisiasa na kiusalama.

Nchini Burundi, mazungumzo ya amani kati ya wapinzani na serikali hayajazaaa matunda. Nchini Sudan Kusini ambayo ni mwanachama mpya wa EAC, vita vimetawala na maelfu wameyakimbia makwao kutokana na mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali.

Licha ya viongozi hao mara kwa mara, kuendelea kusisitiza kuwa wana dhamira ya dhati ya kutekeleza malengo ya Jumuiya kwa manufaa ya wananchi, suala la mkataba wa kibiashara kati yao na Umoja wa Ulaya umeonekana kuwagawa viongozi hawa.

Abdulakrim Atiki mtalaam wa maswala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameiambia RFI kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa ipo katika njia panda kutokana na baadhi ya mataifa kuendelea kukumbukwa na changamoto za kiusalama, kisiasa na suala tata la EPA.

“Hali nchini Burundi sio nzuri sana, demokrasia nchini Uganda ipo mashakani, Rwanda pia hali ni vivyo hivyo kisiasa, na hili ni tatizo,” amesema Atiki.

“Mkataba wa EPA umegawa viongozi wa nchi wanachama, na wameshindwa kuitafsIri kwa manufaa ya wananchi wetu,” ameongeza.

“Bado zinahitajika jitihada zaidi, kuimarisha umoja huu na kila mmoja kuzungumza kwa sauti moja,” amesisitiza Atiki akiwa jijini Dar es salaam.

Inasubiriwa kuona ikiwa mkataba huo utapewa ufumbuzi katika mkutano huo. Mataifa pekee  yaliyoutia saini ni Kenya na Rwanda.

Uganda ilibadilisha uamuzi wake katika dakika za lala salama, huku Tanzania ikisema mpango wake wa kuwa na nchi za viwanda huenda ukaathirika pakubwa  ikiwa itaingia katika mkataba huo.

Burundi nayo ilikataa kuukubali kwa sababu za kisiasa, baada ya Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo vya kiuchumi baada ya rais Piere Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu mwaka 2015.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukishinikiza Mataifa yote ya Jumuiya  kutia saini mkataba huu ili kuondoa vikwazo vya kupata soko la bidhaa zake barani Ulaya, lakini pia bidhaa zake zipate soko la watu Milioni 150 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mataifa mengi ya EAC hayana bidhaa nyingi za kusafirisha barani Ulaya, ukiondoa Kenya ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisafirisha maua katika soko la  Ulaya.

Viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano uliopita
Viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano uliopita wikipedia

Mbali na suala la EPA, Atiki anakiri kuwa kuanza utekelezwaji wa Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja licha ya changamoto mbalimbali, biashara imeanza kuimarika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikwazo vimepungua.

Hata hivyo, utekelezwaji wa wananchi kutoka EAC kuishi na kufanya kazi ndani ya mataifa ya Jumuiya, linasalia kuwa suala lenye changamoto nyingi sana. Kenya na Rwanda tayari imeondoa ada ya kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi lakini Tanzania, Burundi na Uganda bado haijafanya hivyo, jambo ambalo linarudisha nyuma makubaliano yaliyofikiwa.

Kuhusu Shirikisho la kisiasa, mataifa yote yamekubaliana lakini tofauti inayoendelea kujitokeza ni wepesi wa kutekeleza.

Mzozo wa Sudan Kusini, mvutano wa kisiasa nchini Burundi, Somalia kuwa mwanachama mpya wa EAC ni miongoni tu mwa maswala mengine yatakayojadiliwa katika mkutano huo.

Lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya ni kupanua na kuimarisha ushirikiano wa watu wa Afrika Mashariki ili kuharakisha ukuaji wa kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Hata hivyo malengo makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ina nchi 5, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini ni kuhakikisha kuwa kuna Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.