SUDAN KUSINI-UN

UN yasema jeshi la Sudan Kusini limewauawa watu 114 mjini Yei

Mwanajeshi wa Sudan Kusini
Mwanajeshi wa Sudan Kusini chimpreports.com

Umoja wa Mataifa umesema wanajeshi wa serikali nchini Sudan Kusini, wamewauawa raia 114 katika mji wa Yei kati ya mwezi Julai mwaka 2016 na Januari mwaka 2017.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na mauaji hayo, Tume inayoshughulikia maswala ya haki za Binadamu katika Umoja huo imesema  wanawake na wasichana wamebakwa lakini pia mali kuibiwa mali zao na kuteswa.

Watalaam wa Umoja wa Mataifa waliofanya uchunguzi katika mji huo wanasema, mauaji haya yaliegemea ukabila, na yamekuwa mabaya sana kuwahi kutekelezwa na jeshi la serikali katika siku za hivi karibuni.

Hata hivyo, msemaji wa jeshi Kanali Santo Domic Chol ameliambia Shirika la Habari la Uingereza la Reuters kuwa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa sio ya kweli.

Ameongeza kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuishutumu jeshi la nchi yake kwa lengo la kuichafulia jina na kulifanya lionekane ni maadui wa raia wake.

Ripoti hii imekuja baaada ya rais Salva Kiir kumfuta kazi aliyekuwa Mkuu wa majeshi Paul  Malong.

Kumekuwa na madai kuwa alikuwa anaagiza mauaji ya raia wa nchi hiyo.

Mapigano makali yamekuwa yakishuhudiwa nchini humo kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wanaongozwa na makamu wa rais wa zamani Riek Machar ambaye kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini.