TANZANIA-EU

Rais Museveni aitaka EU kuacha vitisho dhidi ya Burundi na EAC

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni DR

Mkutano maalumu wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamatika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, huku viongozi hao wakiutaka umoja wa Ulaya kutoingilia masuala ya ndani ya kwenye nchi za ukanda.

Matangazo ya kibiashara

Akiongea mara baada ya kupokea kijiti cha kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amewaambia viongozi wa umoja wa Ulaya waliohudhuria mkutano huo kucha kuingilia masuala ambayo hayawahusu.

Rais Museveni amesema umoja wa Ulaya ama kwa makusudi au kutokujua mipaka yake umekuwa ukiingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki akitolea mfano vikwazo ambavyo imetangaza dhidi ya Burundi.

Rais Museveni amesema nchi za Afrika na hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinauwezo wa kutatua migogoro yao wenyewe na wasingependa kuona watu kutoka ng’ambo wakitumia utajiri wao na nguvu zao kisiasa kutaka kusuluhisha mgogoro ambao hawajui hata chanzo chake.

“Umoja wa Ulaya tunatatizo na nyingi mnasema mnataka kuiwekea vikwazo Burundi, Burundi ni mwanachama wa EAC, uchumi wa ukanda wetu sio pesa bali ni ushirikiano wa kiuchumi”, rais Museveni aliwaambia ujumbe wa umoja wa Ulaya.

Rais Museveni amesema hauwezi kutaka ushirikiano na nchi wanachama za Afrika Mashariki wakati unataka kuweka vikwazo kwa moja ya nchi ambazo ni mwanachama wao.

“Umoja wa Ulaya na wadau wengine hivi karibuni kulikuwa na mazungumzo kuhusu kuiwekea vikwazo Sudan Kusini katika umoja wa Mataifa...hii ni tabia gani mbaya ambayo umoja wa Ulaya mnayo, mimi ndio naijua Sudan Kusini”. Amesema Museveni.

“Navyoongea sasa nchini mwangu kuna wakimbizi zaidi ya Milioni moja, sasa nyinyi ni akina nani kuzungumzia Sudan Kusini? Hata hivyo nyinyi mnakuja kama watalii tu, sasa mnaanzaje kuzungumzia Burundi au Sudan Kusini? Lazima ukiingia kwenye nyumba ya mtu ugonge hodi na uruhusiwe sio mnaingiaingia tu” alimaliza rais Museveni.

Kuhusu mkataba wa kiuchumi kati ya umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki, rais Museveni amesema nchi hizo haziwezi kuutia saini wakati kuna wanachama wao wengine wanawekewa vikwazo.

Rais Museveni amesema nia ipo ya kutia saini mkataba huo lakini kwa sasa hawawezi kufanya hivyo hadi pale nchi zote zitakapofikia kiwango ambacho wanaona kinafaa na hata Burundi ndio itakapotia saini.