SUDAN KUSINI

Mazungumzo ya amani yaanza nchini Sudan Kusini bila upinzani

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir The Japan Times

Mazungumzo ya kitaifa ya amani nchini Sudan Kusini yanaanza leo baada ya kuahirishwa kwa muda mrefu.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, mazungumzo haya yanaanza bila ya kuwashirisha wanasiasa wa upinzani wanaoongozwa na Riek Machar ambaye anaishi nchini Afrika Kusini.

Juba imeonya kuwa, wapinzani ambao watasusia mazungumzo haya  watachukuliwa hatua kali na hawatavumiliwa.

Daniel Awet Akot, mshauri wa rais Salva Kiir kuhusu maswala ya kijeshi amesema mazungumzo hayo yatafanyika katika majimbo yote ya nchi hiyo kwa lengo la kupata amani ya kudumu ili kumaliza vita vinavyoendelea.

Aidha amesema rais Kiir ameamua kutowasuburi wapinzani ambao wamekuwa wakisema wanaweza tu kushiriki katika mazungumzo hayo ikiwa yataongozwa na kuratibiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Sudan Kusini imekosa amani tangu mwaka 2015, licha ya rais Kiir na aliyekuwa Makamu wake Riek Machar kutia saini mkataba wa amani jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Wanajeshi wa serikali na makundi ya waasi wamekuwa katika makabiliano ya muda mrefu na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, huku mamilioni wakiyakimbia makwao.

Umoja wa Mataifa unasema, wakimbizi nchini humo unahitaji msaada wa haraka wa misaada mbalimbali ya kibinadamu.