SUDAN KUSINI

Waasi nchini Sudan Kusini wasema mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea hayana maana

Kiongozi wa waaasi nchini Sudan Kusini  Riek Machar
Kiongozi wa waaasi nchini Sudan Kusini Riek Machar REUTERS/Goran Tomasevic

Waasi nchini Sudan Kusini wanaoongozwa na aliyekuwa Makamu wa rais Riek Machar amepuuzilia mbali mazungumzo ya kitaifa yaliyoanza hapo jana.

Matangazo ya kibiashara

Machar amesema kinachoendelea ni mbinu ya rais Kiir, kutotaka kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini kati yake na rais Kiir mwaka 2015 jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Akifungua mazungumzo hayo, rais Kiir alitangaza kusitisha vita kati ya vikosi vya serikali na waasi nchini humo, hatua ambayo imekaribishwa na waasi ambao wamesema hata hivyo, wanashuku.

Aidha, alisema kila mtu atashirikishwa katika mazungumzo haya lakini Machar hatakaribishwa binafsi lakini anaweza kutuma wawakilishi wake.

Machar amekuwa akisema kuwa anaweza kushiriki tu katika mazungumzo yatakayoandaliwa na kusimamiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Tangu kuvunjika kwa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini, maelfu ya watu wamepoteza maisha na mamilioni kuyakimbia makwao kwa sababu ya mapigano kati ya wanajeshi na waasi.