KENYA-USALAMA

Polisi wengine wawili wauawa karibu na mpaka wa Somalia nchini Kenya

Madhara yanayosababishwa kutokana na bomu lililotegwa ardhini
Madhara yanayosababishwa kutokana na bomu lililotegwa ardhini kdfintelligencebriefs.

Polisi wawili wameuawa katika Kaunti ya Garrisa Kaskazini Mashariki mwa Kenya baada ya gari walimokuwa wanasafiria kukanyaga bomu lililotegwa ardhini kulipuka.

Matangazo ya kibiashara

Mwakilishi wa serikali katika eneo hilo Mohamud Saleh amethibitisha kutokea kwa mlipuko huo na kusema gari hilo lilikuwa la maafisa wa uhamiaji waliokuwa wanapiga doria na kuelekea katika eneo la Liboi kuisaidia kuimarisha usalama.

Mauaji haya yamekuja siku moja baada ya milipuko mingine miwili kutokea katika eneo la Liboi katika Kaunti hiyo inayopakana na nchi ya Somalia.

Mlipuko wa kwanza ulitokea katika eneo la Liboi Jumatano asubuhi na kusababisha vifo vya Polisi watatu huku mlipuko wa pili ukalenga msafara wa Gavana wa jimbo la Mandera na kusababisha mauaji ya Polisi watano.

Gavana Ali Roba aliyekuwa katika msafara huo aliponea chupuchupu huku walinzi wake wote wakipoteza maisha.

Mashambulizi ndani ya ardhi ya Kenya yalianza mwaka 2011, baada ya jeshi nchini humo kwenda nchini Somalia kupambana na kundu la Al Shabab ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi haya.