KENYA-HAKI

Mahakama ya Haki za binadamu barani Afrika yaitaka Kenya kutoiondoa jamii ya Ogiek msituni

Mmoja wa jamii dogo ya Ogiek nchini Kenya, akielekea nyumbani kwakekatika msitu wa Mau
Mmoja wa jamii dogo ya Ogiek nchini Kenya, akielekea nyumbani kwakekatika msitu wa Mau Yutube

Mahakama ya Afrika kuhusu haki za binadamu yenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania, imeamua kuwa watu wa jamii ya Ogiek wasiondolewe katika Msitu wa Mau nchini Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo uliotolewa Ijumaa jioni, umezua furaha kubwa kwa watu  wa jamii hiyo ndogo ambao wamekuwa wakiishi katika msitu huo Magharibi mwa Kenya kwa muda mrefu.

Mahakama hiyo imeambia serikali ya Kenya, isifikirie kuiondoa tena jamii hiyo ndani ya msitu huo kwa sababu ndio ardhi yao ya asili.

Serikali ya Kenya na ile ya kikoloni kwa zaidi ya miaka 100, zimekuwa zikiwaondoa jamii hii ndani ya msitu na kuwaacha bila makaazi ya kuishi.

Kiongozi wa jamiii hiyo Daniel Kobey ameimbia RFI kuwa uamuzi huo umewapa faraja na furaha kubwa baada ya kuteseka kwa muda mrefu wakihangaishwa na serikali.

“Tuna furaha kubwa sana, tumeumia kwa muda mrefu, shule zimefungwa, watu wamefukuzwa kutoka makwao lakini uamuzi huu umeturejeshea tumaini,” alisema Kobey.

Uamuzi wa Mahakama hiyo ni pigo kwa serikali ya Kenya ambayo ilikuwa inawandoa watu hao kwa lengo la kuhifadhi msitu huo kwa sababu ya mazingira.

Donald Deya  wakili wa jamii hiyo amesema serikali ya Kenya ilishindwa kueleza ni vipi kuishi kwa watu hao ndani ya msitu kulikuwa kunaathiri mazingira na kuongeza kuwa haki za jamii ya Ogiek zimekiukwa kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty Internatonal ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Muthoni Wanyeki amesema uamuzi huo ni wa kihistoria na unatetea haki za jamii hiyo.

Mahakama hiyo imesema serikali ya Kenya ilikuwa inakiuka haki za kabila hilo la Ogiek na sasa ina jukumu la kutii uamuzi wa kutowaondoa katika msitu huo.