TANZANIA-ZANZIBAR

Polisi ya Zanzibar yamsaka kijana aliyejeruhi watu 6 wakiwemo watalii 4

Mji wa kitalii wa Zanzibar wa Stone Town ambako raia wawili wa Uingereza wamemwagiwa tindi kali
Mji wa kitalii wa Zanzibar wa Stone Town ambako raia wawili wa Uingereza wamemwagiwa tindi kali RFI

Polisi visiwani Zanzibar wanaendelea na msako dhidi ya kijana mmoja anayedaiwa kuwajeruhi watu sita kwenye mgahawa mmoja siku ya Jumapili ambapo wanne kati ya waliojeruhiwa ni raia wa Kigeni.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi la Polisi visiwani Zanzibar Hassan Nassir Ali amesema kuwa tukio hili lilitokea Jumapili usiku wakati wakazi wa visiwa hivyo wakiwa kwenye moja ya mgahawa kupata futari.

“Mshambuliaji mwenye umri kati ya miaka 20 na 25 aliingia kwenye mgahawa huo na kuanza kuwachoma visu watu kabla ya kukimbia,” alisema msemaji wa Polisi aliyeoongeza kuwa uchunguzu unaendelea kubaini ikiwa kijana huyo ana matatizo ya akili.

“Tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa kabla hatujatoa taarifa zaidi, hatudhanii kuwa tukio hili lina uhusiano wowote na ugaidi lakini ni baya kwa mustakabali wa sekta yetu ya utalii,” alisema Hassan.

Mashuhuda wa tukio hili wameeleza namna kijana huyo aliyejihami kwa kisu alipoingia kwenye mgahawa wa Lukman mjini Stone Town.

“Baada ya shambulio hili ambalo lilisababisha taharuki ndani ya mgahawa, aliwajeruhi watu wengine wawili wakati akikimbia,” alisema Hassan.

Polisi inasema waliojeruhiwa yumo raia mmoja wa Canada aliyejeruhiwa sehemu ya mdomo na raia wengine wawili wa Ujerumani wenye umri wa kati ya miaka 20 na 24 ambao wote walipata majeraha ya kichwani, mwanamke mmoja raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 66 alijeruhiwa jichoni.

Taarifa zinasema kuwa watalii wengine watatu waliruhusiwa kutoka hospitalini isipokuwa raia wa Ufaransa.

Visiwa vya Zanzibar vimeshuhudia matukio kadhaa ya aina hii ambapo miaka mitatu iliyopita watalii wawili walimwagiwa tindi kali.