KENYA-SIASA

Wagombea nane waidhinishwa kuwania urais nchini Kenya

Rais Uhuru Kenyatta akiidhinishwa na Tume ya Uchaguzi IEBC Mei 29 2017
Rais Uhuru Kenyatta akiidhinishwa na Tume ya Uchaguzi IEBC Mei 29 2017 IEBCKenya

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, imeidhinisha majina ya wagombea wanane kuwania urais mwezi Agosti mwaka huu, wakati wa Uchaguzi Mkuu utakapofanyika.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa wagombea hao, ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya rais Uhuru Kenyatta na mgombea wa muungano wa vyama vya upinzani NASA Raila Odinga.

Hata hivyo, zoezi la mchujo liliwaacha wengine zaidi ya 10 nje ya kinya'nga'nyiro hicho akiwemo Peter Solomon Gichira aliyefikishwa Mahakamani kwa madai ya kutaka kujiua baada ya kuondolewa katika orodha hiyo kwa kutokidhi vigezo.

Ushindani unaotarajiwa kati ya Kenyatta na Odinga, unarejesha nchi hiyo katika historia ya siasa kati ya baba zao, Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa kwanza na Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa Makamu wa kwanza urais baada ya Uhuru mwaka 1963.

Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya katika mkutano uliopita wa kisiasa
Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya katika mkutano uliopita wa kisiasa RailaOdingaK

Hata hivyo, familia hizo mbili zimeendelea kuvutana kisiasa kwa zaidi ya miaka 50 sasa, huku ikikumbukwa kuwa mwaka 2013, Odinga na Kenyatta walimenyana katika uchaguzi ambao Kenyatta alitangazwa mshindi lakini Odinga akadai kuibiwa kura.

Odinga mwenye umri wa miaka 72, akizindua kampeni zake mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema wamejiandaa vya kutosha na ana uhakika wa kushinda mwezi Agosti, huku kipau mbele chake kikiwa ni kupambana na ufisadi.

Kenyatta naye amewaambia Wakenya watazame rekodi ya maendeleo ambayo serikali yake imetekeleza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kutoka Mombasa hadi jijini Nairobi, na kuongeza idadi ya barabara na kumchagua tena.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa na naibu wake William Ruto baada ya kutangaza kuundwa kwa chama kipya cha Jubilee
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa na naibu wake William Ruto baada ya kutangaza kuundwa kwa chama kipya cha Jubilee Kenya State House

Wagombea wengine sita ambao wanatafuta wadhifa huo ni  pamoja na Cyrus Jirongo (UDP), Ekuru Aukot kutoka Thirdway Alliance, Abduba Dida (ARC).

Wagombea binafsi ni pamoja na Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga, ambao wamejinadi kama chaguo sahihi la kuleta mabadiliko.