EAC-SIASA

Kenya yachelewesha kuanza kwa bunge jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EALA yenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EALA yenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania eala.org

Kuanza kwa vikao vya bunge la nne la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA, kumeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni kwa sababu Kenya ambaye ni mwanachama wa Jumuiya hiyo haijatuma wawakilishi wake katika bunge hilo lenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania.

Wabunge wapya wa EALA walitarajiwa kuapishwa siku ya Jumatatu wiki ijayo lakini, msemaji wa bunge hilo Bobi Odiko amesema kwa sasa hilo halitawezekana.

“Tutachelewa kuanza bunge la nne la EALA kwa sababu Kenya bado haijawatuma wabunge wake,” alisema Odiko.

Imekuwa changamoto kubwa kuwapata wawakilishi kutoka nchini Kenya kwa sababu imekuwa ni vigumu kuwapata wabunge bungeni kuidhinisha wawakilishi wanaopendekezwa kwa sababu za kampeni zinazoendelea.

Kuna hofu kuwa huenda wawakilishi Wakenya wasipatikane kwa wakati kwa sababu bunge na Senate nchini humo linatarajiwa kuvunjwa tarehe 15 kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.

Wabunge wa EALA wanataka katika mataifa ya Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Kazi kubwa ya bunge hilo ni kutunga sheria kuendeleza Jumuiya hiyo.