KENYA-MAHAKAMANI

Mawakili nchini Kenya wavutana kuhusu kutangazwa kwa matokeo ya urais

Wapiga kura nchini Kenya mwaka 2013
Wapiga kura nchini Kenya mwaka 2013 iebc

Mawakili wa serikali na upinzani wanachuana vikali katika Mahakama ya rufaa jijini Nairobi, kuhusu suala tata la kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya urais.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi nchini humo IEBC, ilikwenda Mahakamani kutaka uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa matokeo ya mwisho ya urais yatakayokuwa yametangazwa katika maeneo bunge yawe ya mwisho.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umeungwa mkono na muungano wa upinzani NASA, ambao umesema hautashiriki katika uchaguzi huo ikiwa Mahakama ya rufaa itabadilisha maamuzi ya Mahakama ya chini.

Hata hivyo, Tume ye Uchaguzi inasema, kwa sababu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ndiye aliye na uamuzi wa mwisho wa kutangaza matokeo ya urais, ana jukumu la kuyapitia kuhakikisha kuwa yamekamilika kabla ya kuyatangaza.

Wakili wa upinzani James Orengo amewaambia kuna uwezekano mkubwa wa matokeo ya mwisho kubadilishwa na Tume ya Uchaguzi ikiwa, matokeo kutoka maeneo bunge hayataheshimiwa.

Mwanasheria Mkuu wa serikali Githu Muigai na Mawakili wa Tume ya Uchaguzi wamewaambia Majaji wa Mahakama hiyo kuwa, Mwenyekiti wa Tume ambaye kwa sasa ni Wafula Chebukati amepewa mamlaka ya kutangaza matokeo ya mwisho ya urais.

Upinzani pia wamesema matokeo ya urais yanaweza kubadilishwa na Mahakama kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo na sio kupitia Tume ya Uchaguzi.

Majaji Asike Makhandia, Kathurima M'inoti, Patrick Kiage, William Ouko na Agnes Murgor, ndio wanaosikiliza kesi hiyo wakati huu kampeni za kisiasa zikiendelea kushika kasi.

Wachambuzi wa siasa wanasema Majaji hao wana jukumu la kutoa uamuzi utakaoridhisha pande zote za kisiasa na kwa mujibu wa sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.