KENYA-AL SHABAB

Wabunge nchini Kenya watishia kuwanunulia silaha wananchi kukabiliana na Al Shabab

Shambulizi la kigaidi mjini Mogadishu nchini Somalia
Shambulizi la kigaidi mjini Mogadishu nchini Somalia Reuters/Omar Faruk

Wabunge saba nchini Kenya, ambao wanawakilisha maeneo bunge yanayopakana na Somalia wanatishia kuwahami wakaazi wa maeneo yao kwa silaha kupambana na kundi la kigaidi la Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya Habari nchini Kenya vimeripoti kuwa, wabunge hao wakiongozwa na Bare Shill, wamewashtumu maafisa wa usalama kutochukua hatua zozote dhidi ya kundi hili linaloendelea kutishia usalama wa wakaazi wa maeneo hayo.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba, kauli ya wabunge hao waliosema, watanunua silaha hizo kutoka Somalia, ngome ya kundi hilo la Al Shabab.

“Kwanini hamtupi silaha ? Ikiwa hamtaki kutulinda, tutakwenda nchini Somalia na kuzinunua silaha hizo.”

Kaunti za Wajiri, Garrisa na Mandera katika siku za hivi karibuni zimeendelea kushuhudia mashambulizi ya kigaidi, kuwalenga raia wa kawaida lakini pia maafisa wa usalama.

Wanasiasa hao wameishutumu serikali kwa kushindwa kuimarisha hali ya usalama na kuwazuia magaidi wa Al Shabab kuendeleza mashambulizi yao.

Kenya imeendelea kuwa tishio la Al Shabab tangu mwaka 2011, baada ya nchi hiyo kwenda nchini Somalia kupambana na magaidi hayo.