TANZANIA-MIKATABA YA MADINI

Rais Magufuli aagiza mawaziri wa zamani wa wizara ya nishati wachunguzwe

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. 12 Juni, 2017
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. 12 Juni, 2017 Ikulu/Tanzania

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameagiza vyombo vya usalama nchini humo kuwachunguza mawaziri wa zamani wa wizara ya nishati na madini waliotajwa kwenye ripoti ya kamati ya pili ya wanasheria na wachumi, iliyochunguza mchanga wa madini uliozuiliwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Matangazo ya kibiashara

Rais Magufuli amesema haya wakati akipokea ripoti ya kamati ya pili iliyohusisha wachumi na wataalamu wa sheria kuchunguza mchanga wa madini ulioko kwenye makontena yaliyozuiliwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania.

Kamati hii pia baada ya kueleza kwa kina hasara iliyotokana na usafirishaji wa mchanga huu toka mwaka 1999 ilipendekeza mambo 20 ambayo ilitaka Serikali iyafanyie kazi ili kuiepusha nchi na hasara zaidi inayotokana na ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni hayo pamoja na mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi.

Kama ilivyokuwa kwenye kamati ya awali mara baada ya kupkea ripoti hii rais Magufuli alionesha kuchukizwa na namna ambavyo nchi imekuwa ikipoteza mapato huku akiwahoji wale wanaoendelea kupinga harakati zake.

Baada ya kueleza masikitiko yake rais Magufuli akatangaza kuyaunga mkono mapendekezo yote 20 ya kamati huku akitoa maagizo na hatua za kuchukua dhidi ya kampuni ya ACACIA ambayo hata hivoy kwenye uchunguzi wa kamati ilibainika kuwa haina usajili wa kuchimba madini nchini Tanzania.

Uchunguzi huu uliofanywa na kamati ya pili ulitokana na hadidu za rejea iizokuwa imepewa kamati ya awali ambapo zote kwa pamoja zilitakiwa kuchunguza kiasi, aina na thamani ya madini yaliyomo kwenye mchanga uliokuwa usafirishwe kwenda nje ya nchi.