KENYA

Jengo la orofa saba laporomoka jijini Nairobi

Jengo liliporomoka katika mtaa wa Kware, jimboni Embakasi jijini Nairobi
Jengo liliporomoka katika mtaa wa Kware, jimboni Embakasi jijini Nairobi KenyaRedCross

Watu wanne ambao ni mama na watoto wake watatu hawajapatikana baada ya jengo la orofa saba kuporomoka Mashariki mwa jiji kuu la Kenya, Nairobi Jumatatu usiku.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Msalaba mwekundu nchini humo limesema tayari mamia ya watu waliokuwa wanaishi katika jengo hilo wameokolewa.

Msemaji wa kitengo maalum cha uokozi Pius Masai, ameeleza kuwa kufikia mchana, wapangaji 128 walikuwa wameokolewa na kutambuliwa.

Hata hivyo, bado kuna wasiwasi kuwa huenda kuwa idadi zaidi ya watu ambao wamefukiwa na vifusi vya jengo hilo lililopo katika mtaa wa Kware katika jimbo la Embakasi.

Polisi wanasema wakaazi wa jengo walikuwa wameonywa mapema kuhama baada ya nyufa katika kuta za orofa hilo kuanza kuonekana.

Musundi, mmoja wa wakaazi wa mtaa huo ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa la AFP kuwa, kuanguka kwa jengo hilo ni jambo ambalo lilitarajiwa.

Hii sio mara ya kwanza kwa jengo la kupanga kuanguka jijini Nairobi na kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo na majeraha.

Wataalam wa ujenzi wamebaini kuwa wamiliki wengi wa majengo ya kupanga katika jiji hilo, hawazingatii sheria za ujenzi.