UGANDA-CHINA

Uganda yaiomba radhi China kwa madai ya kuhusika na biashara ya pembe za ndovu

Maafisa wa serikali ya Uganda na wenzao wa China jijini Kampala
Maafisa wa serikali ya Uganda na wenzao wa China jijini Kampala

Serikali ya Uganda imeiomba radhi serikali ya China, baada ya Beijing kukataa madai kuwa wafanyikazi wake wawili wanaofanya kazi katika Ubalozi wake jijini Kampala, walihusika katika biashara haramu ya pembe za ndovu.

Matangazo ya kibiashara

Mapema mwezi huu rais Yoweri Museveni alinukuliwa katika vyombo vya Habari nchini mwake, akitaka uchunguzi kufanyika kubaini ukweli wa ushirikiano wafanyikazi hao na wale wa  Shirika la kuhifadhi Wanyama Pori nchini humo baada ya kutowekakwa Kilo 1,300 za pembe za ndovu.

Wizara ya Mambo ya nje ya Uganda imesema inasikitika kwa namna madai hayo yalivyoichafulia jina Ubalozi wa China na kusisitiza kuwa uhusiano wa nchi hizo mbili haujatikiswa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Patrick S. Mugoya amesema baada ya uchunguzi wa kina, wamebaini kuwa taarifa za wajumbe wa ubalozi wa China ambao wamebainika kuwa ni Li Wejin na Yinzhi walikuwa si wafanyikazi wa Ubalozi huo kama wajumbe.

China mwaka uliopita, ilitangaza kuwa kufikia mwisho wa mwaka huu, itapiga marufuku uingizwaji wa pembe za ndovu nchini humo.

Uganda imeendelea kunufaika pakubwa sana na msaada wa kifedha na mkopo kutoka nchini China, kwa lengo la kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama barabara na majengo.