EAC-EALA

Kuanza kwa bunge jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki kucheleweshwa zaidi

Maafisa wa bunge la EALA
Maafisa wa bunge la EALA EALA

Bunge jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA, huenda likaanza baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika nchini Kenya mwezi Agosti mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni kwa sababu hadi kumalizika kwa vikao vya bunge la Kenya hapo jana na kuahirishwa hadi baada ya Uchaguzi Mkuu, vyama vya siasa nchini humo vilikuwa hakijaafikiana kuhusu wabunge watakaohudumu katika bunge la EALA.

Hii inamaanisha kuwa bunge la EALA lenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania, haliwezi kuendelea na shughuli zake kwa sababu mwanachama mmoja ambaye ni Kenya hajatuma wawakilishi wake.

Vyama vya upinzani nchini humo vimewasilisha majina ya wawakilishi wao wanne, lakini upande wa serikali unataka majina saba yawasilishwe ili kuwachagua wanne kati ya hao saba, shinikizo ambazo upinzani umekataa.

                            Soma pia hapa. Bonyeza

Mvutano huu sasa utatatuliwa katika bunge lijalo baada ya Uchaguzi, huku shughuli katika bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiendelea kukwama. Kuwasili kwa wawakilishi wa Kenya, kulitarajiwa kuanza kwa shughuli za bunge hilo kwa kumteua Spika mpya.

Bunge hilo limeahirishwa hadi pale Kenya itakapotuma wawakilishi wake.

Kazi ya bunge la EALA ni kuunda sheria zinazosimamia Jumuiya hiyo inayoundwa na mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.