BURUNDI-UN

Umoja wa Mataifa wabaini raia nchini Burundi wanaendelea kuteswa na vikosi vya serikali

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akiwa amelindwa na wanajeshi
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akiwa amelindwa na wanajeshi Wikipedia

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamebaini kuwa wanajeshi wa Burundi na kundi la Imbonerakure wanaendelea kuwateka, kuwatesa na kuwauwa raia wasiokuwa na hatia nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imesema imebaini hilo baada ya kuchunguza hali ya ukiukwaji wa haki za bindamu katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Hata hivyo, serikali ya Burundi imekanusha madai haya na kusema hayana ukweli wowote.

Balozi wa Burundi katika Umoja wa Mataifa Rénovat Tabu amesema madai hayo yameegemea upande mmoja na wachunguzi hao wamemua kupuuza juhudi za serikali ya Bujumbura kuhimiza amani na usalama.

Hata hivyo, wachunguzi hao wamesema walijaribu mara kadhaa kuiandikia barua serikali ya Bujumbura kuomba ruhusa ya kufika maeneo ambayo ukiukwaji huo unafanyika lakini hawakuruhusiwa.

Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya 700 wamepoteza maisha nchini humo na wengine zaidi ya 400,000 kuyakimbia makwao baada ya kuzuka kwa mzozo wa kisiasa nchini humo mwaka 2015.

Burundi imekuwa ikisema amani imerejea nchini humo.