UGANDA-UNHCR

Kongamano la Kimataifa kuhusu wakimbizi kufanyika jijini Kampala wiki hii

Wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi nchini Uganda
Wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi nchini Uganda Oxfam

Uganda itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu namna ya kuwasaidia wakimbizi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo utafanyika jijini Kampala kati ya tarehe 22 na 23 mwezi huu huu wa Juni.

Wajumbe mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wataungana na rais Yoweri Museveni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress kujadili mbinu mbalimbali za kuwasaidia Mamilioni ya wakimbizi wanaoishi nchini humo.

Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Uganda kwa sasa inawapa hifadhi wakimbizi Milioni 1.2 kutoka mataifa 13 barani Afrika.

Wakimbizi wengi wametokea nchini Sudan Kusini wapatao 900,000, Burundi 50,000, Rwanda 20,000, 44,000 kutoka Somalia na 280,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wengine ni kutokea nchini Sudan na Eritrea.

Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia wakimbizi inasema kila siku, raia zaidi ya 2,000 wanaingia nchini Uganda wakitokea nchini Sudan Kusini.

Raia wa Sudan Kusini wameendelea kuyakimbia makwao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya waasi na vikosi vya usalama. Baa la njaa pia ni sababu kubwa inayosababisha wakimbizi hao kukimbia makwao.

Hii inaifanya Uganda kuwa nchi ya pili inayoongoza kuwapa hifadhi wakimbizi wengi duniani baada ya Uturuki, lakini ya kwanza barani Afrika.

Serikali ya Uganda inasema pamoja na kwamba inatekeleza jukumu lake la Kimataifa la kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani, imelemewa na mzigo wa kifedha wa kuendelea kuwasaidia na sasa inahitaji msaada.

Pamoja na msaada huo, wajumbe hao wanatarajiwa kutembelea kambi mbalimbali za wakimbizi ikiwemo ile ya jijini Kampala, Wilayani Adjumani, Arua na Insingiro kujionea hali ya wakimbizi hao.

Mahitaji muhimu ya wakimbizi nchini Uganda ni pamoja na kuwapa ulinzi, elimu, chakula, dawa na mahitaji mengine kama dawa, makaazi na maji safi ya matumizi.

UNHCR inasema changomoto kubwa imekuwa ni kupata fedha za kuwasaidia wakimbizi kote duniani ambao hadi mwanzoni mwa mwaka 2017, wamekadiriwa kufikia Milioni 65.6 wameyakimbia makwao na mataifa yao kwa sababu mbalimbali, sababu kubwa ikiwa ni machafuko.

Tume hiyo sasa inahitaji msaada wa Dola Bilioni 7.7 kuwasaidia wakimbizi kote duniani.