KENYA-SIASA-UCHAGUZI

NASA kwenda Mahakamani kupinga zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura

Raila Odinga mgombea wa urais kupitia muungano wa upizani NASA akiwa katika kampeni zake mjini Meru hivi karibuni.
Raila Odinga mgombea wa urais kupitia muungano wa upizani NASA akiwa katika kampeni zake mjini Meru hivi karibuni. RailaOdingaKE

Mgombea wa urais kupitia muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, Raila Odinga, amesema muungano huo utakwenda Mahakamani kuzuia zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Dubai kuchapisha karatasi za kupigia kura.

Matangazo ya kibiashara

Odinga ameendelea kusisitiza kuwa kampuni hiyo inayofahamika kama Al Ghurair ilipewa zabuni hiyo kwa upendeleo na Tume ya Uchaguzi na kudokeza kuwa wamiliki wake wamekuwa na ushirikiano wa karibu na rais Uhuru Kenyatta pamoja na familia yake.

Aidha, ameongeza kuwa Tume ya Uchaguzi inapata msukumo kutoka serikalini ili kampuni hiyo iendelee na kazi ya kuchapisha karatasi hizo.

Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa vikali na serikali na kusema hawajali ni kampuni gani itakayopewa zabuni ya kufanya kazi hiyo.

Odinga amekuwa akidai kuwa kampuni hiyo itachapisha karatasi zaidi ili kumsaidia Kenyatta kutangazwa mshindi katika Uchaguzi wa mwezi Agosti.

Soma hapa pia. Bonyeza

Mkurugenzi wa Tume hiyo ya Uchaguzi Ezra Chiloba amekanusha madai kuwa aliwahi kukutana na rais Kenyatta na kukubali kutoa zabuni hiyo kwa kampuni hiyo ya Dubai.

Ameongeza kuwa uchapishaji wa karatasi hizo ni lazima uanze wiki hii kwa sababu ya muda mfupi unaosalia kuelekea siku ya kupiga kura.

Viongozi wa dini wakiongozwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wameitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na haki.