KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Ruto asema madai ya Odinga kuhusu wizi wa kura ni uongo

Naibu rais William Ruto akiwahotubia wafuasi wake jijini Nairobi Juni 20 2017
Naibu rais William Ruto akiwahotubia wafuasi wake jijini Nairobi Juni 20 2017 PHOTO | DPPS

Naibu wa rais nchini Kenya William Ruto na mgombea mwenza wa rais Uhuru Kenyatta kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti, amekanusha madai kuwa chama tawala cha Jubilee kinatumia wanajeshi na Polisi kupanga kuiba kura mwezi Agosti.

Matangazo ya kibiashara

Ruto amesema madai hayo yaliyotolewa na mgombea mkuu wa muungano wa upinzani Raila Odinga, ni ya uongo na hayana msingi wowote.

Ruto amemwelezea Odinga kama mwanasiasa asiyekuwa na ajenda yeyote kwa raia wa nchi hiyo na kuongeza kuwa anapenda sana kulalamika.

“Wanapenda sana kulalamika. Walilalamika kuhusu Makamishena wa Tume ya Uchaguzi, mitambo ya kieletroniki ya kuwatambua wapiga kura, karatasi za kupiga kura na sasa kuhusu jeshi,” alisema Ruto akiwahotubia wafuasi wa Jubilee jijini Nairobi.

Siku ya Jumanne Odinga alidai kuwa wanajeshi wanapewa mafunzo katika kambi ya Embakasi jijini Nairobi na mjini Kakamega Magharibi mwa nchi hiyo kupanga namna ya kuingilia Uchaguzi huo.

Aidha, alionya kuwa kinachotokea ni kama kile kilichojiri mwaka 2007 wakati maafisa wa usalama walipotumiwa kumsaidia Mwai Kibaki kutangazwa mshindi na kuzua machafuko yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja.

Amewataka wanajeshi na maafisa wengine wa usalama kutoshawishika na kujiingiza kwenye siasa na badala yake kufanya kazi yao bila kuegemea upande wowote.

“Tunatoa wito kwa wanajeshi wetu, kuwa waaminifu kwa tamaduni za nchi hii na wasikubali kuingilia maswala ya kisiasa,” alisema Odinga.