KENYA-SIASA-UCHAGUZI-EAC

Uchaguzi wa Kenya ulivyo muhimu kwa nchi za EAC

Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wagombea wakuu wa urais nchini Kenya
Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wagombea wakuu wa urais nchini Kenya DR.

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zinafuatilia kwa karibu kampeni za kisiasa nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni kwa sababu nchi hizi zinaitegemea Kenya kiuchumi, kisiasa na katika masuala ya usalama.

Kenya inayoongoza kiuchumi na katika sekta ya mawasiliano na teknolojia lakini pia miundo mbinu kama viwanja vya ndege na safari za anga, ni muhimu pia kwa mafanikio ya nchi jirani.

Kwa muda mrefu wageni mashuhuri wakiwemo watalii wanaokwenda katika nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekuwa wakifikia jijini Nairobi kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa ya Jomo-Kenyatta kabla ya kuendelea na safari nyingine.

Mambo haya yote, ndio yanazifanya nchi hizo jirani kufuatilia kwa karibu mwendeno wa kisiasa nchini humo na kuhimiza Uchaguzi uwe huru, haki na wa amani ili atakayeshindwa akubali matokeo.

Vigogo wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA.
Vigogo wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA. yutube

Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini kwa muda mrefu zimeendelea kutegemea bandari ya Mombasa kuingiza na kusafirisha bidhaa zake kwa lengo la biashara.

Wakati wa machafuko ya baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007, wafanya biashara walipoteza kiasi kikubwa cha fedha baada ya mali zao kuharibiwa na kuchelewa kufika sokoni.

Hasara hiyo imewafanya wafanyabiashara hao kuendelea kuidai serikali ya Kenya Dola za Marekani Milioni 50 kutokana na uharibifu walioupata.

Mamia ya wakimbizi kutoka nchini Kenya walikimbilia nchini Uganda wakati wa machafuko ya mwaka 2007/8.

Uganda wakati huu inaendelea kukabiliwa na mzigo wa kuwapa hifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Somalia na kuwaongezea wakimbizi wengine kutoka nchini Kenya, itakuwa ni kazi kubwa kwao.

Kenya ni muhimu sana kwa Tanzania kwa sababu ya soko la bidhaa zake ambapo wafanyibiashara kutoka nchi hiyo kubwa ukanda wa Afrika Mashariki, haitaki kupoteza biashara kwa sababu ya machafuko.

Kuhusu usalama, mataifa haya yamekuwa yakishirikiana kwa karibu kupambana na ugaidi ambapo mataifa ya Kenya, Burundi na Uganda yametuma wanajeshi wao nchini Somalia na kuyafanya kutishiwa na kundi hilo la kigaidi ambalo limesababisha mamia ya vifo vya watu na maelfu ya wakimbizi wanaoshi katika kambi ya Daadab nchini Kenya.

Kampeni za Jubilee zikiongozwa na rais Uhuru Kenyatta
Kampeni za Jubilee zikiongozwa na rais Uhuru Kenyatta wikipedia

Kisiasa, inafahamika wazi kuwa rais wa Tanzania John Magufuli ni rafiki wa siku nyingi na wa karibu wa mgombea wa upinzani Raila Odinga lakini licha ya urafiki wao, Magufuli hajajitokeza kuonesha ni nani anayemuunga mkono kati ya Odinga na Kenyatta.

Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani CHADEMA ambacho kimekuwa kikishirikiana kwa karibu miaka iliyopita na Odinga, kimetangaza kuwa kinaunga mkono kuchaguliwa tena kwa rais Kenyatta, kwa kile kilichoeleza kuwa mshirika wao wa siku nyingi (Odinga) alimuunga mkono rais Magufuli wakati wa Uchaguzi mwaka 2015 nchini mwao.

Nchini Uganda, rais Yoweri Museveni ambaye mwaka 2013 alimuunga mkono rais Kenyatta, naye pia hajaweka wazi anayemuunga.

Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa kwa sababu yeye ndio rais mwenye umri mkubwa katika Jumuiya hiyo, na rais Jumuiya ya Afrika Mashariki, angependa kuendelea kufanya kazi na rais Kenyatta anayeweza kumdhibiti kwa urahisi.

Uhusiano wa Museveni na Odinga umekuwa vuguvugu kwa kipindi kirefu na ulionekana kuyumba wakati wanajeshi wa Uganda waliporipotiwa kuwanyanyasa Wakenya katika kisiwa cha Migingo.

Pamoja na uchambuzi huu, wanasiasa hao wawili wamekuwa wakisema kuwa wao ni marafiki ingawa Odinga ameonekana kuwa na urafiki wa karibu na Kizza Besigye, mwanasiasa Mkuu wa upinzani ambaye amekuwa akiwania urais dhidi ya rais Museveni tangu mwaka 2001, 2006, 2011 na 2016.

Mataifa ya Afrika Mashariki yameendelea kutegemeana kisiasa, kiuchumi na katika masuala ya usalama kwa maeneo yao.