KENYA-UCHAGUZI-SIASA

David Maraga: Uchaguzi unapaswa kufanyika Kenya kwa muda uliopangwa

Wabunge wa Seneti nchini Kenya wakionekana wakati wa mjadala wa kupitisha sheria tata ya uchaguzi, 5 Januari, 2017.
Wabunge wa Seneti nchini Kenya wakionekana wakati wa mjadala wa kupitisha sheria tata ya uchaguzi, 5 Januari, 2017. YouTube/Shot/KTN

Jaji Mkuu nchini Kenya David Maraga amesema licha ya muungano wa upinzani kuwasilisha kesi Mahakamani kutaka Tume ya Uchaguzi, kuachana na zabuni iliyotoa kwa kampuni ya Dubai kuchapisha karatasi za kupigia kura, Mahakama itahakikisha kuwa Uchaguzi huo hauahirishwi.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi ilikuwa imeonya kuwa, huenda Uchagizi huo ungeathirika ikiwa, upinzani ungewasilisha kesi hiyo.

Mgombea wa urais kupitia muungano huo Raila Odinga, anasema kampuni hiyo haiwezi kuaminiwa kwa sababu ina ushirikiano wa karibu na familia ya rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa vikali na serikali na kusema hawajali ni kampuni gani itakayopewa zabuni ya kufanya kazi hiyo.

Odinga amekuwa akidai kuwa kampuni hiyo itachapisha karatasi zaidi ili kumsaidia Kenyatta kutangazwa mshindi katika Uchaguzi wa mwezi Agosti.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Ezra Chiloba alikanusha madai kuwa aliwahi kukutana na rais Kenyatta na kukubali kutoa zabuni hiyo kwa kampuni hiyo ya Dubai.

Aliongeza kuwa uchapishaji wa karatasi hizo ni lazima uanze wiki hii kwa sababu ya muda mfupi unaosalia kuelekea siku ya kupiga kura.

Viongozi wa dini wakiongozwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wameitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na haki.