SUDAN KUSINI

Sudan Kusini kutoadhimisha sikukuu ya Uhuru Julai 9

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Goran Tomasevic

Serikali ya Sudan Kusini imesema hakutakuwa na maadhimisho ya siku ya Uhuru tarehe 9 mwezi Julai mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Huu utakuwa ni mwaka wa pili mfululizo kwa nchi hiyo inayoendelea kushuhudia machafuko kutosherehekea siku ya uhuru katika historia ya nchi yake.

Msemaji wa serikali Michael Makuei amethibitisha hilo na kusema  hakuna cha kusherehekea kwa sababu nchi yao inaendelea kupitia wakati mgumu kiusalama.

Sudan Kusini ilijitenga rasmi na Sudan tarehe 9 mwezi Julai mwaka 2011, lakini imekuwa katika vita tangu mwaka 2013 kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.

Machafuko katika nchi hiyo changa duniani, imesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine zaidi ya  Milioni 3.7 kuyakimbia makwao.