KENYA-AFYA

Dawa mpya ya kupunguza makali ya Ukimwi yajaribiwa nchini Kenya

Dawa mpya aina ya DTG kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi
Dawa mpya aina ya DTG kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi REUTERS/Baz Ratner

Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika, kuanza kutumia dawa mpya ya kupambana na virusi vya Ukimwi inayofahamika kama DTG.

Matangazo ya kibiashara

Dawa hiyo mpya inayosaidia mwathirika kuendelea kuishi kwa muda mrefu, ilitengenezwa na kuidhinishwa na Marekani mwaka 2013.

Watalaam wamesema waathiriwa zaidi ya 20,000 nchini Kenya wanapewa dawa hiyo kuona matokeo yake  na baadaye itakwenda nchini Nigeria na hatimaye  nchini Uganda.

Doughtiest Ogutu, mmoja wa watumizi wa dawa hiyo mpya, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa ameamua kutumia hiyo mpya kwa sababu dawa nyingine aliyokuwa anatumia ilikuwa haimsaidii.

“Nimeanza kupata hamu ya kula na sijihisi mchovu tena, amesema Ogutu baada ya kutumia dawa hiyo mpya.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayoendelea kukabiliwa na janga la maambukizi ya Ukimwi.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na maambukizi ya Ukimwi UNAIDS, linalenga kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 90 ya waathiriwa wa virusi hivyo watakuwa wameanza kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.