RWANDA-UCHAGUZI

Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda yamwidhinisha Kagame, wagombea binafsi wakwama

Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa katika mkutano wa RPF hivi karibuni
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa katika mkutano wa RPF hivi karibuni wordpress.com

Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda NEC, imemwidhinisha rais Paul Kagame kutoka chama cha RPF na Frank Habineza kutoka chama cha Democratic Green Party of Rwanda, kuwania urais nchini humo ifikapo tarehe nne mwezi Agosti mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa Tume hiyo Profesa Kalisa Mbanda, ametangaza hilo baada ya wawili hao kukidhi vigezo vyote vinavyohitajika kikatiba.

Hata hivyo, Mbanda amesema wagombea binafsi wameshindwa kukidhi vigezo vyote kuruhusiwa kuwania wadhifa huo.

Tume hiyo sasa imewapa siku tano wagombea hao kuhakikisha kuwa wanatimiza vigezo hivyo la sivyo wafungiwe kushiriki katika Uchaguzi huo.

Kigezo ambacho hawakutimiza ni kutopata sahihi za wapiga kura 600 kutoka kwa wilaya 12 kati ya 30 nchini humo.

Wagombea hao ni pamoja na Gilbert Mwenedata, Diane Shima Rwigara, Philippe Mpayimana na Fred Sekikubo Barafinda.

Tume imewapa hadi tarehe 5 mwezi Julai, kuwasilisha sahihi hizo kabla ya kutangaza orodha ya mwisho ya wagombea urais tarehe 7.

Wagombea binafasi wamekuwa wakilalamikia kusumbuliwa na maafisa wa usalama katika harakati zao za kujitambulisha kwa raia wa nchi hiyo na kueleza mipango yao.