KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Mahakama nchini Kenya yasitisha zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura

Wakenya wakipiga kura katika Uchaguzi wa mwaka 2013
Wakenya wakipiga kura katika Uchaguzi wa mwaka 2013 www.fix.co.ke

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa zoezi la kuchapisha makaratasi ya kupigia kura ya urais lisitishwe na Tume ya Uchaguzi, itangaze upya zabuni ya kufanikisha zoezi hilo.

Matangazo ya kibiashara

Majaji watatu wameeleza kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kubainika kuwa wananchi hawakushirikishwa kikamilifu katika mjadala wa utozaji zabuni kwa kampuni ya Al Ghurair yenye makao yake nchini Dubai.

Katiba ya Kenya inaitaka Tume ya Uchaguzi kuwashirikisha raia katika mdahalo wa utoaji zabuni na kuitangaza kwa kuitangaza katika vyombo vya Habari nchini humo, hatua ambayo Mahakama imebaini kuwa utaratibu huo haukufutwa.

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, ulikwenda Mahakamani kupinga namna zabuni hiyo ilivyotolewa kwa kutowashirikisha wadau wote nchini humo.

Aidha, upinzani umekuwa ukidai kuwa wamiliki wa kampuni hii walikuwa na uhusiano wa karibu na rais Uhuru Kenyatta, jambo ambalo linatoa doa uwazi kuhusu zabuni hiyo, madai ambayo kampuni hiyo na rais Kenyatta wamekanusha.

Uamuzi wa Mahakama umekuja siku 30 kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi ujao, utakaofanyika tarehe 8.

Mawakili wa Tume ya Uchaguzi na kampuni hiyo ya Al Ghurair wamesema watakwenda katika Mahakama ya rufaa, kuitaka kubadilisha uamuzi huo.