KENYA

Kenya yaomboleza kifo cha Balozi wa amani Bethuel Kiplagat

Marehemu Balozi Bethuel Kiplagat  aliyekuwa Mwenyekiti mpya wa tume ya maridhiano nchini Kenya
Marehemu Balozi Bethuel Kiplagat aliyekuwa Mwenyekiti mpya wa tume ya maridhiano nchini Kenya Reuters

Kenya inaomboleza kifo cha mkereketwa wa masuala ya kuhimiza amani Balozi Bethuel Kiplagat.

Matangazo ya kibiashara

Kiplagat amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa anapata matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Atakumbukwa sana kuwa Balozi na afisa wa juu wa serikali ya Kenya.

Pamoja na hilo, aliongoza Tume  ya Ukweli Haki na Mariadhano iliyofanya kazi yake kati ya mwaka 2009-2010 kuchunguza uovu wote uliofanyika nchini humu tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1963 hadi mwaka 2010.

Kiplagat amefariki dunia hata kabla ya mapendekezo ya Tume hiyo ambayo pia ilimtuhumu kuhusika na mauji ya Wagalla alipokuwa afisa wa serikali kuanza kutekelezwa.

Kati ya mwaka 2003-2005 Kiplagat alikuwa mjumbe wa amani katika nchi jirani ya Somalia.

Mwaka 1985-86 alikuwa mratibu wa mazungumzo ya amani nchini Uganda, lakini pia alihusika sana kusaidia kumaliza migogoro nchini Msumbiji, Sudan na Ethiopia.

Aidha, alikuwa Balozi wa Kenya nchini Ufaransa na Uingereza kwa zaidi ya miaka 10.

Rais Mustaafu Daniel Arap Moi amesema anamkumbuka Kiplagat kama mtu aliyefanya bidii kuhakikisha kuwa kuna amani katika nchi za Mataifa ya Afrika Mashariki na kwingineko duniani.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini humo Josephat Nanok amesema Kenya imempoteza mtu aliyejitolea katika maisha yake kupigania amani.

Kiplagat atakumbukwa pia na Radio France International, hasa Idhaa ya Kiswahili kwa kuwa rafiki wa kweli na kuwa tayari kuchambua masuala mbalimbali kuhusu amani.