KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Kampeni zatamatika Kenya tayari kwa uchaguzi

Vinara wa muungano wa upinzanik nchini Kenya, NASA, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, Nairobi, 5 Agosti 2017
Vinara wa muungano wa upinzanik nchini Kenya, NASA, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, Nairobi, 5 Agosti 2017 REUTERS/Thomas Mukoya

Kampeni za kuwania urais katika uchaguzi mkuu nchini Kenya unaotarajiwa kufanyika Jumanne ya wiki ijayo, zimetamatishwa hapo jana kwa vinara wawili wanaopewa nafasi kwenye uchaguzi wa mwaka huu, kuhitimisha kampeni zao kwa kuwataka wananchi kuwa watulivu na kudumisha amani.

Matangazo ya kibiashara

Akifunga kampeni hizo kinara wa muungano wa Upinzani NASA Raila Odinga amewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi kumpigia kura na kuahidi akiingia madarakani ataondoa rushwa ambayo anasema mpinzani wake Uhuru Kenyatta ameshindwa kuiondoa.

Naye Mgombea wa Jubilee na rais wa sasa Uhuru Kenyatta ameahidi elimu bure kwa wakenya wote kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi sekondari na pia kukamilisha miradi ambayo tayari wameianza kama serikali.

Uchaguzi huo unaoangaziwa sana kutokana na mvutano wa kisiasa uliopo baina ya wagombea wawili wanaopewa nafasi kubwa unatarajia kuwa wa amani licha ya wasiwasi uliojitokeza kufuatia kifo cha mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Chriss Msando.

Hali ya usalama inaelezwa kuimarishwa katika jiji kuu la Nairobi na maeneo mengine ambapo kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo takribani askari laki moja na elfu hamsini watasambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura ili kudumisha usalama.