KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Muungano wa NASA wataka Raila Odinga kutangazwa mshindi wa urais

Raila Odinga mgombea wa urais kupitia  muungano wa upinzani NASA
Raila Odinga mgombea wa urais kupitia muungano wa upinzani NASA star newspaper

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, unaitaka Tume ya Uchaguzi nchini humo kumtangaza mgombea wake Raila Odinga kuwa mshindi wa Uchaguzi wa urais.

Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa kiongozi wa muungano huo Musalia Mudavadi amesema wana ushahidi kutoka ndani ya Tume ya Uchaguzi kuwa, Odinga amepata kura Milioni 8, huku mpinzani wake rais Uhuru Kenyatta akipata kura Milioni 7.

Kauli hii imekuja wakati huu, Tume ya Uchaguzi ikiendelea na zoezi la kuhakiki matokeo yaliyotumwa kupitia fomu 34 A na 34 B kutoka maeneo mbalimbali ya bunge na vituo vya kupigia kura.

Aidha, Mudavadi amesema kuwa hawaridhiki na zoezi linaloendelea kuhakiki matokeo hayo ya urais na tayari wameiandikia barua Tume ya Uchaguzi.

Haya yanajiri baada ya NASA kudai kuwa mfumo wa kujumuisha matokeo ya Tume ya Uchaguzi ulidukuliwa, madai ambayo Tume imesema kulikuwa na jaribio hilo lakini halikufaulu.

Katika hatua nyingine, Ekuru Aukot amekuwa mgombea wa pili wa urais kujitokeza na kukubali kushindwa hata kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa.

Japhet Kaluyu na  Cyrus Jirongo pia wamekubali kushindwa.

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, IEBC imesema inatarajiwa kumtangaza mshindi wa Uchaguzi wa urais  siku ya Ijumaa.