KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Waangalizi : Uchaguzi umekuwa mtulivu lakini madai ya upinzani yachunguzwe

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wakitoa ripoti yao jijini Nairobi Agosti 10 2017
Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wakitoa ripoti yao jijini Nairobi Agosti 10 2017 twitter.com/euinkenya

Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya wanataka madai ya Muungano wa upinzani NASA, kuwa mfumo wa Tume ya Uchaguzi IEBC ulidukuliwa na matokeo kubadilishwa, yafanyiwe uchungizi wa kina .

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya Marietje Schaake amesema ni muhimu sana kushughulikia madai hayo ili kuweka kila kitu wazi kuhusu Uchaguzi huu.

“Haya ni madai mazito ambayo tumeyapokea kutoka kwa upinzani na tunataka uchunguzi wa kina kufanyika,” amesema Schaake.

Wito kama huu umetolewa na waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola na wale kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waziri wa zamani wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry, aliyeongoza waangalizi kutoka taasisi ya Jimmy Carter, amesema hatima ya matokeo ya urais yapo katika fomu za 34 A na 34 B zinazohakikiwa na Tume ya Uchaguzi.

"Ukweli wa matokeo haya utabainika baada ya kuhakiki kwa fomu zote kutoka vituoni, tunawapongeza Wakenya kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuonesha ukomavu" amesema.

"Tunalaani mauaji ya Chris Musando, tunataka waliotekeleza mauaji yake wachukuliwa hatua,  lakini pia tunatoa wito kwa wale wanaopinga matokeo kwenda Mahakamani na sio barabarani," ameongeza Kerry.

Mgombea Mkuu wa upinzani NASA, Raila Odinga amesema hayatambui matokeo yaliyotangazwa kwa madai ya wizi wa kura.

Pamoja na hilo, waangalizi hao wamelaani kuuawa kwa Meneja wa Teknolojia katika Tume ya Uchaguzi Chris Msando na kutaka uchunguzi kufanyika na ukweli kubainika.

Wanasiasa nao wameshauriwa kwenda Mahakamani kupinga matokeo ikiwa kutakuwa na utata wowote kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Kuhusu kuuawa kwa watu wanne katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi siku ya Jumatano, na maandamano mjini Kisumu, waangalizi wa Uchaguzi huu wametaka maafisa wa Polisi kuacha kutumia nguvu kupita kiasi.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya, amewapongeza Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi na kupiga kura lakini pia kuendelea kuwa watulivu wakisubiri matokeo ya urais.

“Wakenya wameonesha uvumilivu kwa kipindi kirefu, na tunawaomba wakenya waipe IEBC muda wa kufanya kazi yao na kuwasiliana ipasavyo kwa wananchi,” amesema Schaake.

Rais wa zamani wa Ghana John Dramani Mahama anayeongoza waangalizi wa Jumuiya ya Madola naye amewapongeza Wakenya kwa kuendelea kuwa watulivu wanaposubiri matokeo ya mwisho kutoka kwenye Tume ya Uchaguzi.

“Nawaomba wadau wote waipe Tume ya Uchaguzi muda wa kutosha kushughulikia madai,” amesema Mahama.