BURUNDI-USALAMA

Kundi la vijana wa chama tawala Burundi lashtumiwa kwa unyanyasaji

Wiki za hivi karibuni serikali ya Burundi iliwatolea wito wakimbizi walio uhamishoni kurejea nchini, ikidai kuwa nchi hiyo sasa iko katika amani na salama. Shirika la kimataifa la Haki za Wakimbizi (IRRI) limesema kuwa madai ya serikali ya Burundi ni uongo mtupu.

Polisi wakipiga doria katika moja ya mitaa ya Bujumbura tarehe 12 Aprili 2016.
Polisi wakipiga doria katika moja ya mitaa ya Bujumbura tarehe 12 Aprili 2016. STRINGER / cds / AFP
Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti iliyotolewa Alhamisi, Agosti 24, shirika hili lilikusanya ushuhuda wa Warundi walio uhamishoni. IRRI imelaani vitendo vya unyanyasaji na ukandamizaji vinavyofanyiwa wapinzani na kuushtumu vijana kutoka chama tawala nchini Burundi "Imbonerakure" kuhusika na vitendo hivyo.

"Nilikimbia kwa sababu nilihofia kuuawa," ni jina la ripoti iliyoandikwa na IRRI inayolaani vitendo vya Imbonerakure. kwa mujibu wa Thijs Van Laer, msemaji wa shirika hili, vijana hawa wa chama cha CNDD-FDD wamegeuka na kuwa kile kinachojulikana kama "wanamgambo wa kisiasa": "wanamgambo wameonekana ni wenye vurugu na unyanyasaji dhidi ya wanasiasa wa upinzani na raia wa kawaida ili kuwashinikiza kujiunga na chama tawala. "

IRRI inasema imekusanya ushuhuda kutoka zaidi ya wakimbizi thelathini walio uhamishoni nchini Uganda. Kwa mujibu wa wakimbizi hao, Imbonerakure wamekua wakijihusisha na vitendo viovu nchini kote bila kuwa na hofu ya kuadhibiwa. "Katika baadhi ya wilaya, wamekua wakichukua nafasi yavikosi vya usalama kama vile polisi na idara ya ujasusi. Vile vile wanahusika na kuwkamata watu, kuwaweka kizuizini, kuwatesa na hata kuwatimua nchini au shemu wanakoishi. "

Willy Nyamitwe,Mshauri mkuu wa rais Pierre Nkurunziza katika masuala ya mawasiliano, amesema kuwa ushuhuda huu "umetengenezwa na watuhumiwa ambao walishiriki katika jaribio la mapinduzi na maandamano yasio halali." Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya Warundi 400,000 wametoroka nchi yao tangu kuanza kwa mgogoro wa kisiasa nchini humo.