TANZANIA-UPINZANI

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu apigwa risasi

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu youtube

Mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tanzania Tundu Lissu, amepigwa risasi akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma, polisi wamethibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Chama chake cha CHADEMA kimethibitisha tukio hili lililofanyika Alhamisi mchana wakati mwanasiasa huyo akiwa ndani ya gari lake akitokea bungeni kuhudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea.

Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema, Lissu anaendelea kupata matibabu ya dharura lakini hali yake sio nzuri.

“Tupo hapa Hospitalini, hali yake sio nzuri,” Mbowe aliambia kituo cha Televisheni cha ITV nchini humo.

Madaktari wanaomhudumia wanasema mwanasiasa huyo ambaye pia ni rais wa Chama cha Mawakili cha Tanganyika, amepigwa risasi, tumboni, mgongoni na mguuni.

Mwanasiasa huyu amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya rais John Magufuli na hata amekuwa akimwita “Dikteta”.

Haijabainika ni akina nani waliompiga risasi mwanasiasa huyo.

Viongozi wa serikali mkoani Dodoma wanasema wanachunguza tukio hilo.