KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Mataifa ya nje yawaonya wanasiasa nchini Kenya, Marekani yatishia vikwazo

Maandamano ya muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, dhidi ya Tume ya Uchaguzi IEBC
Maandamano ya muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, dhidi ya Tume ya Uchaguzi IEBC REUTERS/Thomas Mukoya

Viongozi wa siasa nchini Kenya, wanapata shinikizo kutoka nje ya nchi, kuacha kutoa  masharti magumu lakini pia kutoivamia Tume ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi mpya wa urais tarehe 26 mwezi Oktoba.

Matangazo ya kibiashara

Marekani kupitia Wizara ya Mambo ya nje imesema inafuatilia kwa karibu kinachoendelea nchini Kenya, na inahofia matamshi ya mara kwa mara ya uchochezi na kuligawa taifa.

 

Washington DC inataka wanasiasa wa pande zote mbili NASA na Jubilee kuiacha Tume ya Uchaguzi kuendelea na kazi ya kuadaa Uchaguzi.

 

Tayari serikali ya Marekani kupitia Balozi wake nchini humo Robert Godec imeonya kuwa itawawekea vikwazo vya kutokwenda Marekani iwapo  wataendelea na misimamo na kuathiri shughuli za Tume ya Uchaguzi.

 

Wito kama huu, umetolewa na Umoja wa nchi za Ulaya ambao umesema unasikitishwa na matamshi ya kuzua hofu yanayotolewa na viongozi wa siasa nchini humo.

 

Siku ya Jumamosi, serikali ya Ujerumani nayo ilionya kuhusu mchakato wa kubadilisha sheria za Uchaguzi, unaoongozwa na chama cha Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta.

 

Muungano wa upinzani NASA, unaoongozwa na Raila Odinga, umeitisha maandamano kila siku ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi lakini pia kuwashinikiza wabunge wa Jubilee kuachana na mchakato wa kurekebisha sheria za Uchaguzi.

 

Maandamano ya wiki hii, yalifanyika katika miji mikuu nchini humo ya  Nairobi, Kisumu na Mombasa.

 

Hali hii imeendelea kuzua hali ya wasiwasi ya kisiasa kuhusu hatima ya Uchaguzi wa tarehe 26 mwezi Oktoba.