RWANDA-UFARANSA-HAKI

Shambulizi dhidi ya Habyarimana: shahidi mpya ashtumu RPF

Shambulizi dhidi ya ndege ya rais Juvénal Habyarimana (hapa ilikua mwaka 1982) linaonyesha mwanzo wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.
Shambulizi dhidi ya ndege ya rais Juvénal Habyarimana (hapa ilikua mwaka 1982) linaonyesha mwanzo wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. AFP

Mahakama ya Ufaransa ambayo inachunguza shambulio la mwaka 1994 dhidi ya ndege ya rais wa Rwanda Juvénal Habyarimana imeamuru kumsikiliza shahidi mpya ambaye anathibitisha mashtaka dhidi ya utawala wa sasa wa Rwanda pamoja na watu wengine wawili ambao tayari wanachunguzwa, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi James Kabarebe.

Matangazo ya kibiashara

Shahidi huyo amesema kuwa alipewa majukumu ya kuhifadhi makombora mawili ya kudungua ndege, ambayo alisema kuwa yalitumiwakwa kudungua ndege ya rais Juvenal Habyarimana, kwa agizo la kiongozi wake, rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame.

Haijafahamika iwapo ndege ya rais Habyarimana ilidunguliwa kutoka mlima wa Massaka au kutoka mlima wa Kanombe.

Hapa tayari kuna hoja mbili ambazo zinatofautiana. Kwa upande mmoja, inaarifiwa kuwa waasi wa zamani wa Rwanda wa Rwanda Patriotic Front (RPF) wakiongozwa na Paul Kagame, waliokuwa kwenye mlima wa Massaka walipewa agizo kudungua ndege ya Habyarimana.

Kwa upande mwingine, inaarifiwa kuwa makombora yalirushwa dhidi ya ndege ya rais Habyarimana kutoka kilomita 5 na kambi ya kijehi ya Kanombe iliyokua chini ya usimamizi wa jeshi la zamani la Rwanda (FAR), hapa ikimaanisha kuwa Wahutu wenye msimamo mkali walidungua ndege hiyo

Shahidi huyo mpya amesema kuwa alipewa majukumu ya kuhifadhi makombora mawili aina ya SA-16 katika makao makuu ya Waasi wa Kitutsi wa Rwanda wa RPF katika eneo la Mulindi. Shahidi huyo anadai kuwa alizungumza na Frank Nziza na Eric Hakizimana, ambao walirusha makombora hayo dhidi ya ndege ya Habyarimana. Wote wanadai kuwa walirusha makombora hayo kutoka mlima wa Masaka, hali ambayo inahusisha kundi la zamani la waasi la RPF chini ya uongozi wa Paul Kagame. Shahidi huyo mpya, anasema Frank Nziza na Eric Hakizimana walimwambia kuwa makombora hayo yalirushwa akiwepo James Kabarebe. james kabarebe, ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, na Frank Nziza wanachunguzwa tangu mwishoni mwa mwaka 2010.

Mahakama ya Ufaransa inataka kuwakutanisha kwa kuwasikiliza James Kabarebe, Frank Nziza na shahidi huyu mpya, katikati ya mwezi Desemba mwaka huu.

Bernard Maingain, mmoja wa wanasheria wa utawala wa Paul Kagame, amesema shahidi huyu mpya anakuja kuonyesha kutofautiana kwa mahakama ya Ufaransa.