KENYA-AMNESTY INTERNATIONAL

Amnesty International yasema Polisi nchini Kenya wamewauwa wafuasi wa upinzani 33

Polisi nchini Kenya wakikabiliana na waandamanaji wa upinzani jijini Nairobi katika maandamano ya kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi
Polisi nchini Kenya wakikabiliana na waandamanaji wa upinzani jijini Nairobi katika maandamano ya kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi REUTERS/Thomas Mukoya

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty International limetoa ripoti inayoeleza kuwa Polisi nchini Kenya waliwauwa wafuasi wa upinzani 33 kwa kuwapiga risasi.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, watu hao walipoteza maisha mwezi Agosti baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, matokeo ambayo baadaye yalifutwa na Mahakama ya Juu.

Uchunguzi wa Shirika hilo umebaini kuwa ngome za wafuasi wa upinzani ndizo zilizoathiriwa zaidi hasa katika mitaa ya jiji la Nairobi kama Mathare, Kibera, Babadogo, Dandora, Korogocho, Kariobangi, and Kawangware kati ya tarehe 9 hadi 13 mwezi Agosti.

Watafti wa Amnesty wanasema mbali na waandamanaji wengine kupigwa risasi, wengine walipigwa hadi wakapoteza maisha huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Charles Owino, amekanusha ripoti hiyo ya Amnesty International na kusema haina ukweli wowote.

“Watafiti wa Amnesty International, wametoa ripoti ya uongo, polisi hawajasababisha mauaji hayo,” Owino ameiambia runinga ya KTN News nchini humo.

Ripoti hii imekuja wakati huu muungamo wa upinzani NASA ukiendelea na maandamano kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi kuelekea kufanyika kwa Uchaguzi mpya tarehe 26 mwezi huu.