BURUNDI-ICC-HAKI

Burundi yajitoa rasmi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC

Visa vya kukamatwa na ukandamizaji vinandelea kushuhudiwa kwa mwaka mmoja sasa nchini Burundi.
Visa vya kukamatwa na ukandamizaji vinandelea kushuhudiwa kwa mwaka mmoja sasa nchini Burundi. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana

Burundi imejitoa rasmi kwenye mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ikiwa ni mwaka mzima baada ya nchi hiyo kuwasilisha risala yake ya kujitoa kwenye mahakama hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumzia hali hii ya Burundi kujitoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, waziri wa Burundi wa sheria Aimé Laurentine Kanyana, amesema kuwa sio ajabu Burundi kufanya hivyo na haijamanisha kwamba makosa ya jinai ambayo yangeshughulikiwa na ICC ama makosa mengine hayatoadhibiwa akihakikisha kuwa taasisi za sheria Burundi zimejipanga vya kutosha.

Lakini wengi wamekuwa wakijiuliza iwapo ICC bado ina uwezo wa kufungua faili kuhusiana na makosa ya jinahi yaliyotokea nchini Burundi wakati ilikuwa bado mwanachama au la.

Hata hivyo wataalamu wa masuala ya sheria wanasema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ina mamlaka ya kushughulikia makosa yaliyotokea nchini Burundi kabla nchi hiyo haijajitoa kwenye mahakama hiyo. Hayo yamethibitishwa na wakili kutoka Burundi Alexandre Ndikumana.

Burundi imechukuwa hatua ya kujiondoa kwenye mahakama ya ICC kwa hoja kwamba imekuwa ikishughulikia kesi za viongozi wa Afrika pekee na kwamba imekuwa kama chombo cha nchi za magharibi cha kuzikandamiza nchi za Afrika. Hii ilijiri wakati ripoti kadhaa za mashirika ya kimataifa na hata zile za wataalam wa Umoja wa Mataifa zilikuwa zikipendekeza ICC ianzishe uchunguzi kuhusu makosa ya jinai yaliotokea Burundi jambo ambalo lilitupiliwa mbali na viongozi wa Burundi.

Burundi kwa sasa imekua taifa la kwanza kujitoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.