KENYA-UCHAGUZI

Zoezi la kuhesabu kura laendelea Kenya

Ulinzi umeimarishwa wakati huu zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Kenya.
Ulinzi umeimarishwa wakati huu zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Kenya. REUTERS/Siegfried Modola

Siku moja baada ya Wakenya kupiga kura kumchagurais wao mpya, zoezi la kuhesabu kura linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa 11 jioni siku ya Alhamisi Oktoba 26. Kumekuwa na idadi ndogo ya wapiga kura iliyojitokeza kupiga kura, katika maeneo mengi nchini humo kinyume na ilivyotarajiwa mwezi Agosti.

Pamoja na hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati alisema kuwa, zoezi hilo lilikwenda vizuri katika maeneo mengi nchini humo.

Bw. Chebukati amesema ni asilimia 48 ya wapiga kura ndio waliojitokeza.

Wabunge wa upinzani wamekuwa wakizungumza jioni hii na kusema Uchaguzi huo hautafanyika katika kaunti hiyo.

Aidha, wamesema kuwa kwa tathmini yao asilimia 65 ya wapiga kura hawakujitokeza kupiga kura kote nchini.

Hata hivyo uchaguzi huo haukufanyika katika baadhi ya maeneo kutokana na usalama mdogo.

Uchaguzi mpya wa urais wa siku ya Alhamisi Oktoba 26 uligubikwa na makabiliano kati ya waandamanaji wa upinzani n apolisi.

Watu watatu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi na polisi katika ngome za upinzani, katika makabiliano na maafisa wa polisi.

Taarifa kutoka nchini Kenya zinasema mtu mmoja aluawa katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi wakati wafuasi wa upinzani walijaribu kuzuia zoezi la upigaji kura.

Awali vyanzo vya polisi na hospitali Mjini Kisumu vilisema kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 ameuawa huku kijana mwingine akiuawa katika kaunti ya Homa Bay.

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Kenya, Justus Nyangaya ameonya kuwa kuna hatari ya kutokea kwa machafuko zaidi ikiwa hali haitadhibitiwa.

Uchaguzi haukufanyika katika ngome nyingi za upinzani hasa katika Kaunti za Kisumu, Siaya, Homabay na Migori na Uchaguzi huo umeahirishwa hadi siku ya Jumamosi.

Uchaguzi nchini Kenya unafanyika baada ya mahakama ya Juu nchini humo kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali uliofanyika Agosti 8.