BURUNDI-KAFANDO-MAZUNGUMZO

Michel Kafando akutana na viongozi mbalimbali wa Burundi

Michel Kafando, Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi.
Michel Kafando, Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi. AFP PHOTO / FILIPPO MONTEFORTE

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi Michel Kafando yupo jijini Bujumbura, ambapo duru mbalimbali zinaeleza kwamba anakutana na pande mbalimbali zinazohusika na mzozo wa kisiasa nchini Burundi.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumanne alikutana na msuluhishi wa matatizo ya Warundi Edouard Nduwimana, mkutano ambao hata hivyo umefanyika falaghani.

Bw. Kafando anakutana na viongozi mbalimbali mjini Bujumbura, baada ya kukutana na wanasiasa wa upinzani walio uhamishoni nchini Ubelgiji.

Michel Kafando amekua akikutana na wadau mbalimbali nchini Burundi ili kujaribu kutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Burundi imeendelea kukabiliwa na mzigo wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya na Marekani kuishinikiza serikali ya nchi hiyo kuketi kwenye meza ya mazungumzo na upinzani wenye msimamo mkali ulio uhamishoni nje ya nchi.

Hata hivyo serikali ya Burundi imeapa kutoshiriki mazungumzo na wanasiasa walio uhamishoni ikiwataja kuwa walihusika katika jaribio la mapinduzi lililotibuliwa Mei 15, 2015, jaribio ambalo liliongozwa na mshirika wa karibu wa Pierre Nkurunziza, na aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Burundi, Godefroid Niyombare.