KENYA-UCHAGUZI-SIASA

Vyama vya kiraia havikubaliani na matokeo ya uchaguzi mpya Kenya

Polisi wa Kenya wakifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa upinzani. Jumanne, Octoba 24, 2017
Polisi wa Kenya wakifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa upinzani. Jumanne, Octoba 24, 2017 REUTERS/Thomas Mukoya

Muungano wa Mashirika ya kiraia nchini Kenya, umesema matokeo ya Uchaguzi mpya wa urais, sio halali kwa sababu wapiga kura wengi hawakupiga kura.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa mashirika hayo Suba Churchil, amesema kuna umuhimu wa kuundwa kwa serikali ya mpito kwa muda wa mwaka mmoja au miwili ili kuandaliwe kwa Uchaguzi mwingine, utakaokuwa huru na haki.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi wakati ikimtangaza rais Kenyatta mshindi wa uchaguzi huo uliowagawa Wakenya, ilisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Siku ya Jumanne, kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga, alitangaza kutotambua matokeo na uchaguzi huo aliouita wa bandia na kuongeza kuwa muungano huo utaandaa baraza la wananchi litakolokuwa na jukumu la kuandaa maandamano ya amani na kuwahimiza wafuasi wake kususia uchumi, kutoiheshimu serikali katika harakati za kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi mpya.

Tayari mwanaharakati Andrew Okoiti Omtata amekwenda katika Mahakama ya Juu kupinga kuchaguliwa kwa Keyatta na kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa tarehe 10 mwezi huu.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya unasema unatiwa wasiwasi na hali ya kisiasa inayoenelea nchini Kenya na kutoa wito kwa mazungumzo ya kisiasa haraka iwezekanavyo.