KENYA-AFYA-MARBURG

Mlipuko wa ugonjwa wa Marburg: maafisa wa Kenya wafanya uchunguzi Turkana

Wilaya ya Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya inakabiliwa na tishio cha mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.
Wilaya ya Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya inakabiliwa na tishio cha mlipuko wa ugonjwa wa Marburg. RFI

Maafisa wa afya nchini Kenya wanafanya uchunguzi katika mpaka wake na Uganda eneo la Turkana baada ya raia wawili wa Uganda kupoteza maisha karibu na mpaka huo kwa sababu ya ugonjwa hatari wa Marburg ambao dalili zake ni kama za Ebola.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya afya nchini Kenya inasema iko macho kukabiliana na hali hiyo iwapo itaripotiwa na kutoa wito kwa raia wa nchi hiyo wanaoshi mpakani na Uganda, kuripoti visa vyovyote kwa maafisa wa afya iwapo watashuku mtu ameambukizwa ugonjwa huo.

Uganda inakabiliwa na changamoto mpya ya virusi vya Marburg vinavyo ripotiwa mashariki mwa nchi hiyo. Tangu mwezi Septemba uliyopita, watu wawili walifariki dunia kutokana na virusi hivyo vinavyo uwa kwa haraka kama virusi vya Ebola.

Hata hivyo serikali ya Uganda imesema imedhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Hivi karibuni Idara ya utafiti wa virusi vya Marburg nchini Uganda ilihakikisha kwamba ugonjwa huo unauwa haraka kama Ebola. Ni homa inayosababisha mgonjwa kutokwa na damu, kutapika na kuendesha na ugonjwa wenye kuambukia haraka. Ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza miaka 10 iliyopita katika eneo la Kamwenge, magharibi mwa Uganda.

Ugonjwa huu wa Marburg ambao hauna tiba unaweza kumuuwa mtu mwenye afya katika kipindi cha wiki moja tu baada ya kuanza kutapika na kuwa na tumbo la kuendesha na hatimae kutokwa damu ndani kwa ndani.