KENYA-MAANDAMANO-AFYA

Wauguzi wasitisha mgomo wao Kenya

Kenya imekua ikiendelea kukumbwa n amaandamano ya madaktari na wauguzi kwa miezi kadhaa.
Kenya imekua ikiendelea kukumbwa n amaandamano ya madaktari na wauguzi kwa miezi kadhaa. REUTERS/Thomas Mukoya

Wauguzi nchini Kenya hatimaye wamesitisha mgomo wa miezi mitano, baada ya kukubaliana na serikali kuu na zile za Kaunti kuhusu madai yao ya nyongeza ya mshahara na kuboreshewa mazingira ya kazi.

Matangazo ya kibiashara

Huu ndio mgomo uliochukuwa muda mrefu zaidi katika historia ya migomo ya wafanyikazi nchini Kenya, na kusababisha wagonjwa kutaabika na hata wengne kupoteza maisha.

Katibu Mkuu wa chama cha taifa cha wauguzi nchini humo Seth Panyako, amewaambia wauguzi kurudi kazini mara moja na kuwaomba wakenya radhi kwa usumbufu uliojitokeza, kipindi walichokuwa wanagoma

“Kwa mujibu wa Mamlaka niliyopewa na chama chetu, naagiza kumalizika kwa mgomo huu na kuwataka wauguzi kurudi kazini mara moja,” alisema Panyako.

“Tunawaomba radhi Wakenya kwa mateso waliyopata, sio kupenda kwetu tulikuwa tunapambana na mfumo uliokuwa unakaraubuia kuharibika,” aliongeza.

Waziri wa afya Cleopa Mailu, amehiahidi kuwa serikali itatekeleza kikamilifu yale yote waliyokubaliana ndani ya siku 30 na hakuna muuguzi yeyote atakayefutwa kazi, ikiwa ni pamoja na kupata mshahara wote wakati walipokuwa kwenye mgomo.

Baada ya Wauguzi kumaliza mgomo, Wahadhiri wa Vyuo vikuu vya umma nao wameanza mgomo wao kulalamikia kutotekelezwa kwa ahadi waliyopewa na serikali kuwaongezea mshahara.

Wameapa kutorudi kazini hadi pale, malalamiko yao yatakapotekelezwa.