KENYA_USALAMA

Watu watano wathibitishwa kupoteza maisha katika vurugu Nairobi Kenya

Wafuasi wa muungano wa upinzani NASA waandamana kwa kumuunga mkono kiongozi wao Raila Odinga ambaye amerejea Nairobi akitokea Marekani, Novemba 17, 2017
Wafuasi wa muungano wa upinzani NASA waandamana kwa kumuunga mkono kiongozi wao Raila Odinga ambaye amerejea Nairobi akitokea Marekani, Novemba 17, 2017 AFP

Baada ya wiki mbili za utulivu, mji mkuu wa Kenya Nairobi umeshuhudia hali ya sintofahamu jan ijumaa  iliyogubikwa na vurugu, ambapo watu watano wamethibitishwa kuuawa kufuatia makabiliano kati ya wafuasi wa Muungano wa upinzani NASA na maafisa wa kutuliza ghasia nchini Kenya waliokua wakizima maandamano ya upinzani, yaliyopigwa marufuku na serikali.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi George Kinoti watano hao walipigwa kwa mawe na watu wenye hasira katika matukio tofauti baada ya kudaiwa kukamatwa wakiiba kinyume na madai ya kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Hata hivyo mpiga picha wa shirika la habari la AFP anasema aliona miili ya vijana watatu waliopigwa risasi, huku polisi wakitawanya maandamano ya upinzani katika maeneo matatu ya mji wa Nairobi ikiwa ni pamoja na Muthurwa.

Maelfu ya wafuasi wa upinzani waliingia mitaani katika mji mkuu wa Kenya kwenda kumlaki kiongozi wao Raila Odinga, ambaye alirejea kutoka Marekani. Bw Odinga amelaani ukimya wa nchi za magharibi kwa mchakato wa uchaguzi nchini Kenya.

Wafuasi wa muungano wa upinzani NASA kwanza walikusanyika nje ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, kusherehekea kurudi kwa Bw. Odinga, mwenye umri wa miaka 72, wakipiga kelele wakisema "Baba, Baba, Baba", jina lake la utani.

Umati wa watu, hasa vijana, walianza kufuata msafara wa Raila Odinga, ambaye alitarajia kuhutubia wafuasi wake katika eneo moja mjini Nairobi.

Lakini polisi waliingilia kati na kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi, huku risasi zikifyatuliwa hewani. Wakati huo huo waandamanaji walirusha mawe na hali kuwa mbaya zaidi.