KENYA-MAHAKAMA-SIASA

Kesi ya kupinga ushindi wa rais Kenyatta yatupiliwa mbali

Jaji Mkuu wa Kenya  David Maraga (Katikati) akiwa na Majaji wenzake wa Mahakama ya Juu
Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga (Katikati) akiwa na Majaji wenzake wa Mahakama ya Juu Photo: Reuters/Baz Ratner

Mahakama ya Juu nchini Kenya, imetupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa rais Uhuru Kenyatta baada ya Uchaguzi wa mwezi Oktoba.

Matangazo ya kibiashara

Jaji Mkuu David Maraga amesema kuwa, uamuzi huo uliafikiwa kwa pamoja na Majaji wote sita baada ya kusikiliza kesi hiyo wiki iliyopita.

Wapiga kura wawili Njonjo Mue na Khelef Khalifa pamoja na mwanasiasa wa zamani Harun Mwau, walikwenda Mahakamani, kupinga ushindi wa rais Kenyatta.

“Tumeafikiana kwa pamoja kuhusu uamuzi huu, kuwa kesi hii haikuwasilishwa vema na hivyo tumeitupilia mbali,” alisema Jaji Maraga.

“Tutakuja kutoa maelezo kamili ya kwanini tumefikia uamuzi huu, ndani ya siku 21,” aliongeza Jaji Maraga.

Wakili wa wapiga kura wawili waliokwenda Mahakamani, Harun Ndubi, amesema ameshangazwa na uamuzi huo kwa kile alichokieleza kuwa, waliwasilisha ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Kenyatta hakushinda kwa haki.

“Nimeshangazwa sana na uamuzi huu, lakini tunasubiri kusikia kwa kina kuhusu ni kwanini walifikia uamuzi huu,” amesema Harun Ndumbi.

Naye wakili wa rais Uhuru Kenyatta Ahmednassir Abdullahi amesema uamuzi wa Mahakama ni ushindi mkubwa kwa haki nchini humo.

“Huu ni ushindi mkubwa, haki imetendeka na sasa haya mambo yamekwisha,” alisema Ahmednassir.

Baada ya uamuzi huu, rais Kenyatta anatarajiwa kuapishwa kuongoza kwa muhula wa pili siku ya Jumanne wiki ijayo.

Wafuasi wa chama cha Jubilee wamekuwa wakisherehekea uamuzi wa Mahakama ya Juu.