RWANDA-AU-LIBYA-WAHAMIAJI

Rwanda yakubali kuwapokea wahamiaji 30,000 wa Afrika kutoka Libya

Wahamiaji wa Cote d'Ivoire waliorejeshwa nchini kutoka Libya wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Abidjan, Jumatatu, Novemba 20, 2017.
Wahamiaji wa Cote d'Ivoire waliorejeshwa nchini kutoka Libya wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Abidjan, Jumatatu, Novemba 20, 2017. REUTERS/Luc Gnago

Serikali ya Rwanda imesema iko tayari kupokea wakimbizi 30,000 wa Afrika kutoka Libya. Rwanda imejibu wito kutoka Umoja wa Afrika kufuatia suala la soko la watumwa nchini Libya.

Matangazo ya kibiashara

"Kutokana na falsafa ya kisiasa ya Rwanda na historia yetu wenyewe, hatuwezi kusalia kimya wakati binadamu wanadhulumiwa haki yao wanateswa na kuuzwa kama ng'ombe," amesema waziri wa kigeni wa Rwanda, kwa mujibu wa BBC kitengo cha Afrika (BBC Afrique).

Waziri wa Mashauriano ya Kigeni wa Rwanda, Louise Mushikiwabo alikua akijibu wito wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ambaye aliomba msaada kutoka nchi za bara la Afrika katika kukabiliana na hali hii nzito inayowakabili wahamiaji wa kiafrika.

Rwanda inakuwa nchi ya kwanza kuitikia wito huu kwa kupendekeza kupokea wahamiaji 30,000 wa Afrika kutoka Libya.

Habari kuhusu visa vya kuuzwa kwa wahamiaji kama watumwa ilifichuliwa na kituo cha televisheni cha CNN Novemba 14, kikionyesha "soko la watumwa" nchini Libya, hali ambayo imesababisha hasira duniani.