KENYA

Raila Odinga akataa shinikizo la kuapishwa Jumanne

Kiongozi wa Muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Kiongozi wa Muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga REUTERS/Thomas Mukoya

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Nasa, Raila Odinga jana Jumamosi alikataa shinikizo la wafuasi wa muungano huo kutaka kumwapisha siku ya Jumanne, siku ambayo rais Uhuru Kenyatta anatarajia kuapishwa kuongoza taifa la Kenya kwa muhula wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano wa mashauriano uliodumu kwa saa tano katika kaunti ya Machakos, inasemekana kuwa Odinga ametoa wito wa tahadhari, akielezea taswira yake ya kimataifa, na heshima yake kwa sheria na Katiba ambayo wengi katika umoja huo anasema yeye ni mwanzilishi.

Hata hivyo kuna changamoto halisi ya kisheria katika ukweli kwamba ni uhaini kula kiapo cha urais na Odinga ameepuka hilo akisema kwamba Jumanne itakuwa siku ya kuomboleza vifo vya watu waliouawa na polisi.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya ambaye alijiondoa kwenye uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 baada ya kufanikiwa kushinda katika pingamizi la ushindi wa rais Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 08 kwa madai ya kukosekana kwa mageuzi ya uchaguzi, ameuita uchaguzi wa marudio bandia na kutoa wito wa uchaguzi mpya chini ya tume mpya ya uchaguzi.